Msongo wa mawazo
Ni kawaida kwa vijana kuwa na huzuni au kuwa na mabadiliko ya hisia. Miaka hii huwa na changamoto. Mara nyingi uko kati ya kuwa mzee sana kufurahia mambo uliyozoea kufanya - na mchanga sana kufanya mambo unayotaka. Kila kitu kinabadilika.
Inaweza kuwa vigumu kutambua msongo wa mawazo kwa vijana. Watu walio na msongo wa mawazo wanaweza:
- Kuhisi huzuni, kulia, mabadiliko ya hisia au wepesi wa hasira
- Kuhisi 'utupu' au 'kufa ganzi', aghalabu hali hii huwa mbaya zaidi asubuhi
- Kutopata tena furaha katika mambo ambayo hapo awali yaliwafurahisha
- Kuwa na milipuko ya hasira
- Kujiona hawana thamani au ni wenye hatia, na wanajilaumu. Wanaweza kusema mambo kama vile, ‘ni kosa langu’ au ‘mimi nimeshindwa’
- Kuacha kuonana na marafiki
- Kuwa na mawazo hasi ambayo hayawatoki, ikiwa ni pamoja na mawazo kuhusu kujiumiza au kujiua. Wanaweza kufikiria au kusema mambo kama vile, ‘maisha hayana thamani tena’ au ‘Siwezi kufanya haya tena’.
Msongo wa mawazo unaweza pia kusababisha dalili za kimwili kama vile:
- uchovu, kupungua kwa nguvu na motisha
- mabadiliko katika hamu ya kula au uzani
- matatizo ya kimwili yasiyo wazi au yasiyoeleweka - kwa mfano, maumivu ya tumbo na kichwa
- matatizo ya kulala - kwa mfano, ugumu wa kupata usingizi au kulala
Watu walio na msongo wa mawazo mara nyingi huwa na ugumu wa kumakinika, kufanya maamuzi, kutatua matatizo, au kukumbuka habari.
Kwa kawaida, ili kutambua kama una msongo wa mawazo unahitaji kuonekana na mtaalamu mwenye mafunzo mwafaka. Unaweza kupata mtaalamu kupitia nyenzo hizi za afya ya akili.