Tuzungumze Kuhusu Ridhaa
Ridhaa ni neno ambalo unaweza kuwa umesikia wakati wa kuzungumzia ngono na mahusiano.
Ridhaa ni pale mtu anapokubali jambo kwa uwazi na kwa furaha, na hajashinikizwa kwa vyovyote kutoa jibu lake. Ridhaa ni kitu ambacho unahitaji kuomba, na kupokea, kila wakati unapokuwa na aina yoyote ya shughuli za ngono. Ngono bila ridhaa ni unyanyasaji wa kijinsia au ubakaji.
Ridhaa ni muhimu kwa sababu inahusu jinsi tunavyowasiliana na kuangalia kwa makini hisia za kila mmoja wetu, na inatusaidia kufanya tu mambo ambayo yanakubalika kwetu na pia mtu mwingine. Ridhaa ni mazungumzo yanayoendelea. Iwapo mtu ataomba ridhaa yako, hilo ni jambo zuri - kuwa na ujasiri na sema jinsi unavyohisi. Ikiwa unaomba ridhaa ya mtu mwingine, kila wakati heshimu jibu lake ikiwa atasema 'hapana'. Kumbuka kwamba ‘hapana’ inamaanisha ‘hapana’; usijaribu kuwashawishi!
Mtu ambaye yuko kimya, anatabasamu tu au anasikika kama hana uhakika na ni kama anajaribu kukufurahisha bado hajatoa ridhaa yake. Ikiwa mtu atakubali kufanya ngono kwa sababu anashinikizwa na vitendo vya kuogofya, vitisho au vurugu, au ni mlevi - bado hajatoa ridhaa kwa uhuru.Ridhaa:
Ridhaa ni:
- Ni chaguo ambalo uko huru kufanya bila shinikizo au kulazimishwa.
- Ni 'ndiyo' ya kweli na haiwezi kutolewa ukiwa umelewa, umetumia dawa za kulevya au umelala.
- Hutolewa wakati mtu ana habari zote na anajua kisa chote. Kwa mfano, ikiwa mtu atasema kuwa atatumia kondomu kisha asiitumie, hakuna ridhaa kamili.
- Huzungumziwa katika kila hatua na kuridhia jambo moja hakumaanishi kuwa umeridhia kila jambo.
- Ni unapofanya tu mambo unayotaka kufanya, sio mambo ambayo unahisi unatarajiwa kufanya.
- Haidumu. Mtu anaweza kubadilisha mawazo yake kuhusu kushiriki ngono na kuondoa ridhaa yake wakati wowote, hata kama aliwahi kushiriki ngono na mtu huyo hapo awali, na hata kama tayari yuko uchi au kitandani na mtu fulani.
Ikiwa hujatoa ridhaa yako na umepitia unyanyasaji wa kijinsia au ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na ubakaji, hili si kosa lako. Si muhimu kama ulikuwa peke yako na mtu mwingine, au ulikuwa nje usiku, na haijalishi ni nini ulikuwa umevaa. Huna lawama. Wasiliana na 116/1195 ili upate usaidizi na msaada unaohitaji.