Mabadiliko ya hali ya hewa huathiri ubora na wingi wa maji
Kote duniani, kupungua kwa rasilimali za maji safi kunahatarisha afya na maisha. Kufikia mwaka wa 2020, mabadiliko ya hali ya hewa yanatarajiwa kupelekea watu milioni 75 katika bara la Afrika pekee kupata ongezeko la matatizo ya maji.
Maji safi ni muhimu kwa maisha, afya na upataji wa riziki. Mabadiliko ya hali ya hewa yanatarajiwa kuleta ukame zaidi, mafuriko na kufurika kwa bahari, jambo ambalo litafanya upatikanaji wa maji safi na yasiyo na chumvi kuwa mgumu zaidi. Kuongezeka kwa uchafuzi, uvutaji mkubwa wa maji kwenye tabaka la maji na uharibifu wa maeneo ya vyanzo za maji kunaifanya hali ya hatari kuwa mbaya zaidi. Wakati huo huo, uchafuzi kutoka kwa viwanda, kilimo na usimamizi usiofaa wa taka za binadamu unahatarisha vyanzo vya awali vya maji safi.
Wakati maji safi yanayopatikana ni kidogo, huenda watu wakayahifadhi kwa minajili ya kunywa na kutumia maji kidogo kuosha mikono na kuzingatia usafi. Maji machafu na usafi wa mazingira duni unaweza kusababisha magonjwa. Aidha, ukosefu wa maji unaweza kusababisha migogoro, watu wakilinda rasilimali zao, na kuongezeka kwa uhamiaji, watu wanapohamia mahali ambapo maji yanapatikana.
Usimamizi wa makini wa huduma za maji na usafi wa mazingira ni muhimu. Njia na teknolojia mpya zinapaswa kusitawishwa ili kutumia vizuri na kulinda rasilimali za maji. Kusafisha maji tena na kuyatumia tena kunaweza kuwa sio tu kwa gharama nafuu, lakini ni muhimu.