Kukaa Salama
Kukaa salama kunamaanisha kujitunza na kuwatunza wengine. Tunapokua, jinsi tunavyofikiri, kuhisi na kuuona ulimwengu hubadilika. Tunakuza utambulisho wetu, kuanzisha aina mpya za uhusiano na kujaribu vitu mbalimbali. Ni wakati ambao unajisikia huru, jasiri na kwamba hakuna kitu kinachoweza kukudhuru, lakini kuna mambo ambayo yanaweza kukuweka hatarini na ni vizuri kujua jinsi ya kujilinda.
Shinikizo la rika
Marafiki ni muhimu sana lakini wakati mwingine wanaweza kujaribu kutufanya tufanye mambo ambayo hatutaki kuyafanya au tunayojua kwamba hatupaswi kuyafanya. Ikiwa hufurahii hali fulani, amini hisia zako na uondoke.
Uyanyasaji wa kijinsia
Kutoa kauli zinazohusiana na ngono kwa sauti ya juu au 'kumzomea' mtu ni unyanyasaji wa kijinsia na ni aina ya dhuluma za kijinsia. Jambo la kusikitisha ni kwamba wasichana na wanawake wengi hupitia aina hii ya dhuluma kila siku. Linaweza kuwafanya wahisi woga, hasira, na huzuni. Watu hawapaswi kufanywa kuhisi hivi na jambo hili litakoma tu ikiwa sote tutashutumu aina hii ya tabia.
Ikiwa uko pamoja na kikundi cha marafiki wanaowazomea watu, ni rahisi kutosema lolote, lakini kimya chako kinawaambia wengine kwamba kuzomea watu ni sawa na kinakufanya uwe ‘mtazamaji’ - mtu anayetazama lakini hafanyi chochote. Usiwe mtazamaji!
Pombe na dawa za kulevya
Watu wengi hutumia pombe na dawa nyinginezo za kulevya kwa ajili ya kujifurahisha au kuwafanya wajisikie vizuri. Kunywa pombe ukiwa mchanga wakati ubongo wako bado unakua kunaweza kuwa na madhara. Wakati mwingine pombe na dawa zingine za kulevya zinaweza kuwafanya watu kuwa wachokozi, wenye hasira, na hata wenye vurugu, hasa ikiwa wazinatumia kwa wingi. Zinaweza pia kusababisha maamuzi mabaya kuhusu ngono na mahusiano. Ikiwa una wasiwasi kuhusu utumiaji wako - au wa rafiki - wa pombe au dawa za kulevya, zungumza na mtu anayeweza kukusaidia.
Kupitia vurugu
Kuona au kukumbana na vurugu nyumbani au kutoka kwa wenzi ni jambo la kufadhaisha sana. Kila mtu ana haki ya kujisikia salama na hapaswi kamwe kuhisi anatishwa au hana salama, hasa nyumbani kwake (pata maelezo zaidi kuhusu umuhimu wa mahusiano mazuri). Vijana wenye ulemavu wanaweza kuwa katika hatari zaidi ya kuwa kwenye mahusiano ya vurugu au ya unyonyaji kwa hivyo ni muhimu sana kuwa waangalifu. Ukikumbana na vurugu za aina yoyote, pata usaidizi ili kuhakikisha kuwa wewe na wanafamilia wengine mko salama na ili ukusaidie kukabiliana na hali hiyo. Hata wakati wa UVIKO-19 usaidizi huu unapatikana.