Ni nini hufanyika wakati wa hedhi?
Mzunguko wa hedhi ni nini?
Mzunguko wa hedhi huanza katika siku ya kwanza ya hedhi yako na huisha wakati wa kuanza kwa hedhi inayofuata. Unaitwa mzunguko kwa sababu kwa kawaida unajirudia.
Wakati wa mzunguko, homoni (kemikali katika mwili wako) huongezeka na kupungua, na kusababisha mabadiliko mengine ya mwili.
Mzunguko mzima wa hedhi unaweza kudumu kati ya siku 21 na 35, lakini kwa wasichana na wanawake wengi, mara nyingi urefu hubadilika kutoka mzunguko mmoja hadi mwingine, na hubadilika jinsi miaka inavyosonga.
Kila mtu ni tofauti, na mabadiliko katika mzunguko wako ni jambo la kawaida. Wasichana wanapoanza kupata hedhi, mara nyingi mzunguko wao wa hedhi haufuati utaratibu unaotabirika. Hedhi inaweza kuja mwezi mmoja na isije mwezi unaofuata, au zikaja zikiwa zimetengwa na wiki chache tu.
Kitu gani hufanyika wakati wa hedhi?
- Mzunguko wa hedhi huanza na hedhi yako, ambayo hudumu muda wa kama siku 2-7.
- Katika sehemu ya kwanza ya mzunguko wa hedhi, yai kwenye ovari huanza kukomaa na utando (au kuta) za uterasi huanza kuwa mzito kwa damu na tishu.
- Wakati yai liko tayari, linaachiliwa kutoka kwa moja ya ovari (hii inaitwa 'uovuleshaji') na kushuka chini kupitia kwa mrija (unaoitwa 'mrija wa fallopia') kuelekea kwa uterasi.
- Ikiwa yai halitarutubishwa, damu na tishu zinazozunguka uterasi hazihitajiki na humwagwa kupitia uke, ambalo ndilo jambo unalopata wakati wa hedhi yako.
Je, sehemu za mzunguko wa hedhi ni zipi?
Mzunguko wa hedhi una sehemu mbili kuu: kabla ya uovuleshaji na baada ya uovuleshaji.
Kabla ya uovuleshaji huanza na siku ya kwanza ya hedhi na kuishia na uovuleshaji.
Wakati wa hedhi, mayai yaliyo katika ovari yanaendelea kukomaa. Kwa kawaida ni moja tu linalokomaa kabisa. Wakati yai limekomaa, linaachiliwa kutoka kwa ovari. Hii inaitwa uovuleshaji. Wasichana na wanawake wanaweza kushika mimba kwa takriban siku tano kabla na siku moja baada ya uovuleshaji.
Urefu wa kabla ya uovuleshaji hutofautiana sana kati ya wanawake na kutoka kwa mzunguko mmoja hadi mwingine. Kwa kawaida huwa na urefu wa kati ya siku 13-18 lakini unaweza kuwa mfupi kama siku 8 au mrefu kama wa siku 31, kulingana na muda wa mzunguko wako wa hedhi.
Sehemu ya pili ya mzunguko, baada ya uovuleshaji, huanza baada ya uovuleshaji na kumalizika siku moja kabla ya hedhi yako inayofuata kuanza. Kwa kawaida hudumu siku 10-15, lakini inaweza kuchukua kutoka siku 6 hadi 16.
Je, ni lini ni rahisi kupata mimba ukushiriki ngono?
Unaweza kupata mimba wakati wowote unapojamiiana bila kizuia mimba, lakini kuna uwezekano mkubwa wa wanawake kupata mimba siku 2-3 baada ya uovuleshaji. Pata maelezo zaidi kuhusu mbinu za kuzuia mimba na uzazi wa majira.
Je, yai huishi muda gani baada ya uovuleshaji?
Yai huishi tu kwa saa 12-24 baada ya uovuleshaji. Baada ya yai kufa kwenye mrija wa fallopia, mwili hilifyonza, isipokuwa kama limerutubishwa na manii.
Inamaanisha nini nikikosa hedhi?
Wakati mwingine unaweza kukosa au kuruka hedhi bila sababu yoyote, hasa katika miaka michache ya kwanza ya hedhi yako. Unaweza kufuatilia mzunguko wako kwa kuhesabu siku kuanzia wakati hedhi yako inapoanza, hadi inapofika tena. Ikiwa una simu mahiri na intaneti, unaweza kufuatilia hedhi yako kupitia programu ya OKY.
Mambo mengine ambayo yanaweza kuathiri mpangilio wa hedhi yako ni:
- mfadhaiko
- dawa
- baadhi ya njia za kuzuia mimba
- chakula, hasa ikiwa kinakufanya uwe mwembamba sana
- kufanya mazoezi kupita kiasi
- kusafiri.
Ikiwa msichana ameshiriki ngono bila kutumia njia ya kuzuia mimba (kizuia mimba), kukosa hedhi ni ishara kwamba anaweza kuwa mjamzito.