101

Maelezo ya Msingi kuhusu Hedhi

Nitapata lini hedhi yangu ya kwanza?

Muda wake unabadilika, lakini wasichana wengi huanza kupata hedhi kati ya umri wa miaka10 na 15

Hedhi yangu itadumu kwa muda gani?

Kwa kawaida, hedhi huchukua kati ya siku mbili na saba lakini hutofautiana kulingana na wasichana. Iwapo hedhi yako itadumu kwa zaidi ya siku saba, mwambie mzazi, mwalimu wa kike, muuguzi au daktari.

Nitapoteza damu kiasi gani?

Huenda ikaonekana kuwa nyingi, lakini huwa takribani vijiko vitatu kwa jumla.

Je, nitavuja kiwango sawa cha damu kila siku ya hedhi?

Hapana. Utavuja damu nyingi siku ya kwanza ya hedhi na hupungua hadi itakapoisha kabisa baada ya siku kadhaa. Hii inamaanisha kuwa utahitaji vifaa vingi vya hedhi siku ya kwanza ikilinganishwa na siku ya mwisho.

Itakuwaje iwapo sina kifaa cha hedhi na niko mbali na nyumbani?

Iwapo mwalimu au rafiki wa kike hawezi kukusaidia, unaweza kukunja karatasi ya shashi pamoja ili utengeneze sodo ya muda na uiweke kwenye chupi yako. Hii haitadumu kwa muda, lakini inaweza kukusaidia kabla ya kupata kifaa kinachofaa.

Je, watu watajua kuwa ninapata hedhi?

Hapana. Hakuna atakayejua kuwa unapata hedhi kwa sababu hakuna dalili zinazoonekana kuhusu hedhi kwa mtu yeyote. Hata hivyo, ni vizuri umwambie mwanafamilia au rafiki ikiwa ni mara yako ya kwanza kupata hedhi na unahitaji usaidizi.

Ninaweza kuenda shuleni na kushiriki michezo?

Ndiyo! Hakuna sababu ya kukosa kuenda shuleni au kuacha kushiriki michezo kama kawaida. Hakikisha tu kuwa umebeba vifaa vya hedhi iwapo utahitaji kuvibadilisha ukiwa shuleni.

Bado sijaanza kupata hedhi! Nitafanya nini?

Hakuna anayefanana na mwingine na miili yetu hukua katika viwango mbalimbali. Hili si tatizo na unaweza kuzungumza na mwalimu wa kike akusaidie uelewe kinachotendeka. Tunakushauri umwone daktari tu ikiwa umefikisha umri wa miaka16 na hujaanza kupata hedhi; iwapo kipindi chako cha hedhi kitadumu kwa zaidi ya siku saba au ikiwa hedhi itaanza na kukoma kwa ghafla.

Kuna tofauti gani kati ya sodo zinazoweza kutupwa na padi za nguo?

Sodo zinazoweza kutupwa hutumika mara moja kisha kutupwa, lakini padi za nguo zinaweza kusafishwa na kutumika tena wakati zimekauka.

Je, ninahitaji kumwona daktari wakati ninaanza kupata hedhi?

Hapana. Kupata hedhi ni jambo la kawaida.

Sipati hedhi mara moja kwa mwezi kama wasichana wengine. Nitafanya nini?

Usijali. Katika mwaka wa kwanza au wa pili baada ya kupata hedhi ya kwanza, huenda hutaweza kutabiri kipindi cha hedhi yako. Hii ni kwa sababu mwili huchukua muda kuafikiana na hali hiyo. Pia, kumbuka kuwa baadhi ya wasichana hupata hedhi kila baada ya siku 21 na wengine kila baada ya siku 35. Kwa wastani, wasichana hupata hedhi kila baada ya siku 28.

Iliyotangulia Ifuatayo